Unordered List

Definition List

Mauaji Ya Mfanyakazi Wa TBC Yafunguka Zaidi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura.
MAJAMBAZI  wanne wakiongozwa na mwanamke juzi usiku walifunga barabara ya Ubungo Maziwa jijini Dar es Salaam na kupora Sh. 600,000 kwa mfanyabiashara wa duka la vyakula kisha kumua dereva la Shirika la Utangazaji (TBC) na kumjeruhi jirani kwa kumpiga risasi sehemu za makalio.


Dereva aliyeuawa ametajwa kwa jina la Ramadhani Giza, mkazi wa Gongolamboto na majeruhi alifahamika kwa jina la Mwarami Mshana mkazi wa Ubungo Maziwa. Akisimulia tukio hilo, Hamdan Rajabu ambaye aliporwa fedha hizo pamoja na vocha za simu zenye thamani ya Sh. 400,000 alisema majambazi hao walifika mtaani hapo usiku wakiwa na bunduki na moja kwa moja walimfuata dukani na kumuaru awape fedha.

Alisema wakati akitoka nje ya duka lake mlangoni alikutana na jambazi moja na kumwamuaru arudi ndani ya duka na kumpa fedha haraka. Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa hivyo alishikwa na butwaa na ghafla jambazi huyo alimtolea bastola mbili na bunduki moja iliyokatwa kitako na kumtaka alale chini kifudifudi.

Rajabu alisema baada ya kuona hali imekuwa ngumu, alilazimika kutii amri na kulala na kwamba aliambiwa atoe fedha zote za mauzo ya siku hiyo.

“Niliambiwa niwape fedha  na wakati huo jambazi mwingine alikuwa ameingia ndani na hivyo kufanya idadi ifikie wawili na niliwaambia wafungue droo na kuchukua chochote watakachokikuta humo na ndipo walipofungua na kukusanya mauzo yote yaliyofikia Shilingi laki sita,” alisema.

Alisema kabla ya kumaliza uporaji huo, waliona gari la TBC alilokuwa akiendesha marehemu ambalo lilikuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara likiwasha taa na kuonyesha dalili za kuondoka ndipo jambazi mwanamke alipomfyatulia risasi na kumuua papo hapo.

Mashuhuda wa tukio hilo waliongea na paparazi wetu kuwa tukio hilo lilikuwa kama sinema kwa kuwa kila jambazi alikuwa akifanya kazi yake kwa umakini huku madereva waliokuwa wamewabeba majambazi hao wakiwa wamebaki kwenye piki piki bila kuzizima.

Majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kwamba hali yake inaendelea vizuri.

 Marehemu alikuwa kwenye gari lenye namba za usajili STK 355 Toyota Land Cruiser mali ya shirika hilo lililokuwa limeegeshwa karibu na eneo la tukio akiwa na mwanamke aliyefahamika kwa jina la Mwanakombo Daud (41), mfanyabiashara na mkazi wa eneo la Ubungo maziwa.

 Katika  tukio hilo majambazi hayo yalimjeruhi kwenye kiuno Mharami Rajabu (25) ambaye ni dereva wa gari kenye namba za usajili T.404 BLZ Mitsubish Fuso aliyekuwa ameegesha gari eneo hilo la tukio.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura, alisema dereva huyo aliuawa na majambazi wanne ambao walivamia duka la Namanga Shopping Center linalomilikiwa na Hamdan Rajabu (45).

Wambura alisema majambazi hao walifanikiwa kupora vocha za simu zenye thamani ya Sh. 400,000 na fedha taslimu na kwamba wakati wote wa tukio hilo la uporaji likiendelea  jambazi mwanamke ndiye alikuwa kiongozi wao wa kulinda eneola nje.

Alisema kufuatia tukio hilo, Polisi wanaendelea  na msako mkali wa kuwasaka wahalifu wanaojihusisha na ujambazi wa kutumia silaha, unyanganyi wa kutumia nguvu, wauzaji wa madawa ya kulevya pamoja na uhalifu mwingine.

Habari kutoka gazeti la Nipashe
Mauaji Ya Mfanyakazi Wa TBC Yafunguka Zaidi Mauaji Ya Mfanyakazi Wa TBC Yafunguka Zaidi Reviewed by Admin on Friday, November 08, 2013 Rating: 5

No comments:

Tunapenda kuyasoma maoni/reaction kutoka kwako!

Kama una maoni tofauti na chapisho la hapo juu, wasiliana nasi kupitia ukurasa wetu wa mawasiliano

Powered by Blogger.