Unordered List

Definition List

Askofu Anaswa Na Dawa Za Kulevya Thamani Ya Bilioni Mbili

Stori: MAKONGORO OGING’ na Haruni Sanchawa


KIMENUKA! Vigogo wa madawa ya kulevya wakiwemo viongozi wa dini sasa wanaanza kupukutika kutoka kwenye mstari wa siri huku baadhi yao wakikimbilia nje ya nchi kufuatia oparesheni kali inayofanywa na Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulenya Tanzania kuwanasa kila kukicha, Uwazi lina mchoro kamili.

Hivi karibuni kikosi hicho kimemkamata askofu (mwangalizi mkuu wa kanisa) aliyetambulika kwa jina la Emeka Nwachukwu Mert raia wa Nigeria ambaye ana kanisa la kiroho maeneo ya Sinza jijini Dar. Jina la kanisa hilo limedhibitiwa na vyombo husika kwa sababu ya uchunguzi zaidi na uhalali wake wa kuwepo nchini.

SIKU YA TUKIO
Vyanzo vyetu makini ndani ya kikosi kazi vinaeleza kwamba, mchungaji huyo alikamatwa Oktoba 31, mwaka huu saa kumi usiku Tegeta wilayani Kinondoni, Dar es Salaam akiwa na madawa ya kulevya ‘unga’ aina ya heroine kilo 35.

KAMA UNGEINGIA SOKONI
Habari za ndani kutoka kwenye oparesheni hiyo zinasema kuwa, endapo unga huo ungeingia sokoni na kununuliwa, basi mtumishi huyo wa Mungu angevuna kitita cha zaidi ya shilingi bilioni mbili.

NYUMBA ALIYONASIWA YA PROFESA
Mchungaji huyo ambaye serikali imeanza kazi ya kulichunguza kanisa lake, alidakwa na mzigo huo haramu kwenye makazi aliyopanga ambayo ni nyumba ya profesa mmoja wa chuo kikuu, Mbezi jijini Dar es Salaam.

WASHIRIKA NAO WADAKWA
Kwa mujibu wa chanzo, kamatakamata ya mchungaji huyo pia iliwakumba watuhumiwa wengine ambao ni Walyat Khan raia wa Pakistani, Chuksi Sylvester Agbazuo na Tony Olafor wote raia wa Nigeria na inadaiwa kwamba walikuwa wakikamatwa maeneo mbalimbali na kutoroka.

HABARI NYETI
Habari za siri ambazo Uwazi ilizinasa zinadai kuwa, watumishi wa Mungu waliokuwa kwenye orodha ya kunaswa walikuwa wengi lakini wamekimbilia nje ya nchi na kikosi hicho kimeshawasiliana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kwa ajili ya kuwasaka na kuwatia nguvuni.

MAJINA MAPYA MEZANI KWA NZOWA
Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya Tanzania, SACP Godfrey Nzowa amekabidhiwa majina ya vigogo wakiwemo viongozi wa dini ambao ni sugu katika biashara hiyo. Mbali na majina hayo, pia amepewa ratiba zao za safari za kibiashara hivyo kilichobaki ni kuwafuatilia na kuwakamata na ushahidi ili kuhakikisha kwamba hawawezi kupona mahakamani.

MTANDAO HATARI
Habari zaidi zinadai kuwa, siku za hivi karibuni, Kamanda Nzowa amekuwa akifumua mtandao wa watu wazito katika biashara hiyo na imebainika kuwa vigogo hao wana mtandao mkubwa serikalini ikiwemo wizara ya mambo ya ndani ambao wanawalinda kwa kupewa mamilioni ya pesa kwa ajili ya usimamizi wa upitishwaji wa biashara hiyo haramu kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar. “Unajua zamani viongozi hao serikalini walikuwa wakimsumbua Kamanda Nzowa ili awaachie watuhumiwa waliokamatwa na unga bila mafanikio, lakini sasa wameshamsoma kiasi kwamba hata wakikamatwa hawampigii simu tena,” kilisema chanzo kingine.

WATOTO WA VIGOGO
Habari nyingine zinadai kuwa, Kamanda Nzowa pia ana majina ya watoto wa vigogo wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo na anayafanyia kazi.

KUMBUKUMBU
Kukamatwa kwa askofu huyo kumekuja baada ya kukamatwa kwa vigogo ambao ni viongozi wa dini katika makanisa ya kilokole. Januari 11, mwaka huu, Askofu Moris Charles alidaiwa kukamatwa na polisi maeneo ya Chinga Mbili mkoani Lindi akiwa na kilo 210 za madawa ya kulevya ainaya heroine yenye thamani ya shilingi bilioni 9.4, kesi yake bado inaendelea mahakamani mkoani humo. Juni 8, 2011 polisi walifanikiwa kumkamata Mchungaji Kapupu Denis Okechuku wa kanisa la kilokole lililopo Kinondoni Biafra akiwa na kilo 81 za cocaine, kesi yao bado ipo Mahakama ya Kisutu, Dar.

KAMANDA NZOWA
Uwazi lilipomtafuta Kamanda Nzowa ofisini kwake juzi, alisema kuna watu wanne waliokamatwa Tegeta wakiwa na kilo 35 za madawa ya kulevya aina ya heroin na kuna wengine wanatafutwa kuhusiana na tukio hilo.“Kwa sasa nisingependa kuzungumzia sakata hilo kutokana na sababu za kiupelelezi kwani kuna wengine tunawatafuta na nitahakikisha wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, nawashukuru wananchi kwa ushirikiano wao,” alisema Nzowa.
Chanzo: GPL
Askofu Anaswa Na Dawa Za Kulevya Thamani Ya Bilioni Mbili Askofu Anaswa Na Dawa Za Kulevya Thamani Ya Bilioni Mbili Reviewed by Admin on Tuesday, November 11, 2014 Rating: 5

No comments:

Tunapenda kuyasoma maoni/reaction kutoka kwako!

Kama una maoni tofauti na chapisho la hapo juu, wasiliana nasi kupitia ukurasa wetu wa mawasiliano

Powered by Blogger.