Unordered List

Definition List

Mwananchi: Dawa Za Kuzuia Ugonjwa Wa UKIMWI Zatumiwa Vibaya Kama Njia Mbadala Ya Kondomu

 
Dar es Salaam. Wanawake wanaofanya biashara ya kuuza miili na wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja sasa wanatumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi aina ya Truvada kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo badala ya kutumia mipira ya kondomu.

Mwananchi lilizungumza na baadhi ya wafanyabiashara ya ngono jijini katika maeneo ya Mwananyamala Hospitali, Komakoma na Vingunguti ambao walisema kuwa wanatumia dawa hizo kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya VVU ili kuwaridhisha wateja wasiopendelea mipira hiyo.

Baadhi ya wafanyabiashara hao walidai kuwa wanatumia Truvada kuzuia maambukizi pindi wanapokutana na wanaume wakware ambao huwabaka au kuwalazimisha kufanya mapenzi bila kinga.
“Hizi dawa tunazipata katika hospitali na wakati mwingine katika maduka makubwa ya dawa. Kwa sababu zinazuia maambukizi ya Ukimwi na sisi ni watu ambao tunafanya kazi katika mazingira hatarishi,” anasema Leyla Musa, mmoja wa wanawake hao.

Si hivyo tu, kwa kuwa hii ni biashara baadhi yao hukubali kufanya mapenzi bila mipira ili kupata fedha nyingi kutoka kwa wanaume.

Wengine hukimbilia huduma ya PEP
Baadhi ya wanawake hao wanasema kuwa baada ya kufanya mapenzi na wanaume kadhaa asubuhi huenda katika kliniki zinazotoa huduma za ARV na kudanganya kuwa wamebakwa na kisha hupewa huduma za dharura za ARV zinazoitwa kwa kitaalamu Post-exposure prophylaxis.
Kwa kawaida mtu aliyebakwa au kujikata hupewa dawa aina ya Lamivudine, Zerophidine au Truvada kulingana na uzito wa tatizo.

“Tunatumia hizi dawa mara kwa mara lakini tunafanya hivyo katika kliniki tofauti ili tusigundulike,” alisema mmoja wao, mkazi wa Mwananyamala, Mariam Leshaniki.
Kwa maelezo ya Dk Rachel Baggaley, mtaalamu wa masuala ya Ukimwi wa Shirika la Afya Duniani anasema dawa za PEP zipo maeneo mengi duniani kwa sasa na zinafanya kazi kwa ufanisi pia hazina madhara kwa mwanamke.

“Dawa hizi siyo sumu mwilini, zinaingia kwenye mfumo wako wa damu kabla virusi havijajizatiti na inavizuia ili mradi uzitumie ndani ya saa 72,” anasema Dk Baggaley.

Dawa ya Truvada, ambayo ina mchanganyiko wa dawa aina ya Tenovofir na Emtricitabine, imethibitishwa kuwa salama kwa kupunguza makali ya VVU pia kuzuia maambukizi mapya. Dawa hizi zinazotengenezwa nchini India, zimekuwa msaada mkubwa wa tiba kwenye nchi zinazoendelea.

>>> Mwananchi
Mwananchi: Dawa Za Kuzuia Ugonjwa Wa UKIMWI Zatumiwa Vibaya Kama Njia Mbadala Ya Kondomu Mwananchi: Dawa Za Kuzuia Ugonjwa Wa UKIMWI Zatumiwa Vibaya Kama Njia Mbadala Ya Kondomu Reviewed by BkuHabari Admin on Sunday, May 18, 2014 Rating: 5

No comments:

Tunapenda kuyasoma maoni/reaction kutoka kwako!

Kama una maoni tofauti na chapisho la hapo juu, wasiliana nasi kupitia ukurasa wetu wa mawasiliano

Powered by Blogger.